Kaimu mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha Dkt. Yusuph Mhando (wa kwanza kulia) akimuongoza Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula (wa 2 kushoto) kutembelea majengo yanayojengwa Kampasi ya Kikuletwa.

Kaimu mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha Dkt. Yusuph Mhando akimuongoza Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula kutembelea majengo yanayojengwa Kampasi ya Kikuletwa.

Chuo cha Ufundi Arusha Kampasi ya Kikuletwa kimepongezwa kwa hatua nzuri ya ujenzi iliyofikiwa kwenye Kampasi hiyo iliyopo Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro ambayo inatarajiwa kuwa kituo cha umahiri katika nishati jadidifu.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Frankline Rwezimula alipotembelea Kampasi hiyo ili kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo mbalimbali yanayojengwa pamoja na kusikiliza changamoto.

“Ninawapongeza Chuo cha Ufundi Arusha kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa usimamizi, nawapongeza wakandarasi, na kuna wakandarasi wazawa wawili na wanafanya kazi vizuri, Wizara ya Elimu itaendelea kutoa ‘support’ kwa vyuo vya ndani ili viweze kujitegemea na kushindana kimataifa” alisema Dkt. Rwezimula.

Aidha Dkt. Rwezimula ameeleza kwamba baada ya Kampasi hiyo kukamilika itasaidia kutoa wataalamu ambao watasaidia kupunguza matumizi ya mkaa na kuni na kuleta nishati ambayo itakua rafiki kwa mazingira.

Kampasi ya Kikuletwa inajengwa kwa ufadhili wa benki ya Dunia kupitia mradi wa Afrika mashariki wa kujenga ujuzi na uingiliano wa kikanda (EASTRIP) ambao utaiboresha Kampasi hiyo kuwa kituo cha umahiri katika nishati jadidifu.